AJIRA ZA WALIMU NA MJADALA UNAOENDELEA CHUONI: JE BEDCP NA BEDPSY HAZITAMBULIKI?
Ni mjadala unaoshika kasi ghafla baada ya waziri wa
elimu na mafunzo ya ufundi Dk. Shukuru kwambwa kutangaza nafasi za ajira kwa
walimu,suala hasa sio tu ajira kutangazwa bali ni mgawanyo wa fursa hiyo kwa
kada mbalimbali za ualimu.Lengo la makala ya hii si kujadili kiwango cha
asilimia za kupanda au kushuka kwa uajiri katika tasnia ninayoiheshimu ya
ualimu bali kuthamini namna ambavyo walimu wanafunzi waliopo vyuoni
walivyopokea fursa hizo za wenzao, lakini hasa nitalilenga kundi la wakufunzi
la wanasihi na wanasaikolojia hususani katika chuo kikuuu Teofilo Kisanji.
Hofu imetanda kuwa wanafunzi wa ushauri na
saikolojia hawawezi kuajiriwa chini ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi,hili
limekuja baada ya wanafunzi toka TEKU kutopata nafasi ya kazi hata mmoja kwa
wale waliosomea kozi hizo,hoja ni kwamba je serikali haitambui kozi hizi? Au
upya wa kozi hapa TEKU ndio chanzo?. Pamoja na kwamba ni maswali magumu yasiyo
na majibu ya moja kwa moja pia tunapaswa kufanya utafiti wa kina juu ya sababu
zilizoleta hali hii.
Kwa upande wangu nitajenga hoja mbili tu kuhusiana
na suala hili alafu nitakaribisha mjadala.Hoja ya kwanza ni kwamba suala la
wahitimu wakufunzi kukosa fursa za ajira linaigusa TEKU tu,tujiulize vipi
kuhusu vyuo kama UDSM,SEKUCO,TUMAINI,UDOM
n.k. hapa tujenge swali la mjadala kwamba wahitimu kutoka vyuo hivyo
wamepata nafasi hizo zinazolalamikiwa? Kama jibu ni hapana basi kuna haja ya
kumtafuta mchawi.Pia hapa kuna jambo ambalo limeibuka kuwa kozi hizi
hazitambuliwi na serikali…mimi sio msemaji wa wizara lakini nachoweza sema ni
kwamba huu ni aina ya upotoshaji wa kijinga kabisa na kwa utafiti wangu
niliofanya kwa kuchunguza ‘post’ za ualimu za miaka miwili nyuma ni kwamba
wahitimu wakufunzi walipata ‘post’ za serikali ila kwa kuwa TEKU ilikuwa bado
haijatoa wahitimu wa kozi hizi ndio maana haikuwa ‘stori’.
Hoja yangu ya pili ni kwamba kukosa kwa ‘post’ kwa
wahitimu wakufunzi wa ualimu kutoka vyuo mbalimbali nchini na TEKU ikwemo iwe
changamoto kwa wanafunzi waliobaki vyuoni na waweze kusoma alama za nyakati
kuwa kuajiriwa kunategemea pia na vipaumbele vya serikali kutokana na mahitaji,
hivyo basi waondokane na fikra mgando za kukaa na kusubiri ‘post’ kipindi
wanapokuwa wamemaliza vyuo badala ya kujihusisha na shughuli nyingine hata
kutafuta kazi kwenye taasisi mbalimbali zinazoshughulika na masuala
waliyosomea.
Kuhitimisha niseme kwamba natambua kuwa kwa mfumo
wetu serikali ndio mwajiri nambari moja kuhusu suala la ajira lakini pia
tutambue kuwa changamoto katika soko la ajira ni pana sana vilevile ongezeko la
vyuo vikuu limeongeza idadi ya wataalam katika kada yetu ya ualimu basi sisi
walimu wa kisasa tuwe na fikra pambanuzi na kujiandaa kuendana na kupambana na
soko la ajira ndani hata la kimataifa.
Nakaribisha mjadala.
Imeandaliwa na; Melkiory John
TEKU/BEDCP/101562
0655141602/0767141603
No comments:
Post a Comment